Thursday, August 7, 2014

Kinana: Msiwajadili Warioba, Ukawa



kinnana_52726.jpg

Dodoma. Katika jitihada za kuliepusha Bunge la Katiba kupoteza mwelekeo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewataka wajumbe wake kuacha kumjadili mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) waliosusia vikao vya Bunge hilo.
Badala yake, CCM imewaelekeza wajumbe hao kujadili "mambo yanayowahusu wananchi" ambayo yamependekezwa katika Rasimu ya Katiba.

Maelekezo hayo yalitolewa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alipokutana na wajumbe wa Bunge Maalumu ambao ni wabunge wa Jamhuri ya Muungano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na wale walioteuliwa kuingia katika Bunge hilo kupitia wajumbe wa kuteuliwa na Rais kupitia kundi la 201.

Kikao hicho ambacho kilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa CCM Makao Makuu, pamoja na mambo mengine pia kiligusia mwenendo wa Bunge la Katiba, huku Kinana akitoa maelezo mafupi kuwahakikishia msimamo wa chama hicho kwamba kinaunga mkono hatua za kuendelea kwake katika awamu ya pili.

Maelekezo hayo yamekuja baada ya wajumbe hao kutumia muda mwingi wa siku ya kwanza ya awamu ya pili ya Bunge la Katiba, kuwashutumu wajumbe wa Ukawa kwa kususia vikao, wakiwaeleza kuwa mwafaka unaweza tu kupatikana ndani ya chombo hicho cha kuandika katiba.

Wajumbe hao walidiriki hata kutafuta mfumo wa kuwazuia wajumbe hao wa Ukawa kuzungumzia Katiba wakiwa nje ya Bunge Maalumu.

Habari kutoka ndani ya kikao hicho ambazo gazeti hili lilizipata zinasema wajumbe hao walimwomba Kinana kuwa Ukawa na Jaji Warioba wazuiwe kujadili Katiba nje ya Bunge.

Kinana, akijibu hoja hiyo katika kikao hicho kilichokuwa chini ya uenyekiti wa Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema wajumbe hao wa CCM hawapaswi kulumbana na watu walioko nje ya Bunge na asingependa kusikia wakiwataja Ukawa wala Warioba wakati wakichangia bungeni.

Kadhalika Kinana alisema chama hicho hakiwezi kushawishi kuzuiwa kwa mikutano wala mijadala inayoendeshwa nje ya Bunge Maalumu la Katiba.

Gazeti hili lilidokezwa kuwa suala hilo la wajumbe wa Ukawa na Jaji Warioba lilitawala mjadala kwa dakika kadhaa kutokana na baadhi ya wajumbe kupinga mawazo ya kukaa kimya, lakini Kinana aliwaambia kwamba kama wanataka kujibizana na Ukawa au watu wanaozungumza kwenye midahalo, iwe maeneo mengine, akisema Bunge si mahali pake.

"Alisema kama tunataka kuwajibu Ukawa na wengine, basi tuandae midahalo au mikutano ya hadhara na kwamba bungeni ni mahali pa kujadili mambo muhimu tena siyo yanayohusu watawala, bali yanayowahusu wananchi," kilisema chanzo chetu kikimkariri Kinana.

Kinana akizungumza na gazeti hili juzi usiku, alithibitisha kuzungumza na wabunge wa CCM lakini hakutaka kuingia kwa undani kuhusu kile kilichojiri katika mkutano wake.

Hata hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikiri kwamba Kinana alitoa maelekezo kuwa Bunge Maalumu litumike kwa ajili ya mijadala ya mambo ya wananchi na siyo kulumbana na watu walioko nje ya Bunge hilo.

"Kweli katibu mkuu alikuwa na kikao cha wabunge na hilo ni moja kati ya mambo mengi ambayo yalizungumzwa," alisema Nape lakini alikataa kuingia kwa undani kuhusu suala hilo.

Katika siku ya kwanza ya awamu ya pili ya Mkutano wa Bunge Maalumu ambao ulitumika kwa ajili ya marekebisho ya Kanuni za Bunge hilo, baadhi ya wajumbe waliwashambulia Ukawa kwa kutorejea bungeni tangu waliposusia vikao hivyo Aprili 16, mwaka huu.

Kadhalika wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akiwamo Jaji Warioba walishambuliwa hasa kutokana na mdahalo walioufanya Jumatatu wiki hii, walipotoa ufafanuzi wa masuala kadhaa ambayo yamekuwa kiini cha mgogoro kuhusu Katiba hiyo.

Katika kikao hicho, baadhi ya wajumbe walinukuliwa wakisema kuwa chanzo cha mijadala isiyo na tija ni wabunge wengi kutosoma taarifa mbalimbali ambazo zingewawezesha kufanya uchambuzi wa kina kuhusu Katiba, hivyo wamekuwa wakijenga hoja zao kwenye msingi dhaifu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani alinukuliwa akionyesha moja ya nyaraka ambazo zingewasaidia wajumbe hao kujenga hoja zenye mashiko, lakini akasema hicho hakitokei kwa sababu wajumbe hawana utamaduni wa kujisomea.
Utoro wa mawaziri.

Suala jingine ambalo lilizua mjadala mkubwa ndani ya kikao hicho ni kuhusu mawaziri kutohudhuria vikao vya kamati, hali ambayo inasababisha kukosekana kwa akidi ya kutosha kupitisha baadhi ya ibara muhimu za Rasimu ya Katiba.

"Miongoni mwetu wapo waliokuwa wakali sana wakisema mawaziri wanapuuza mchakato huo kwani mahudhurio yao hayaridhishi, maana hata katika Bunge lililopita baadhi ya mambo yalikwama kwa kukosekana kwa kura mbili au tatu na hapo unakuta mawaziri ambao ni wajumbe hawapo," kilifafanua chanzo hicho.

Mwenyekiti wa Kamati namba 11 ya Bunge Maalumu, Anne Kilango Malecela alinukuliwa akitoa mfano wa kamati yake ambayo ina wajumbe watano ambao ni mawaziri na kwamba ikitokea wote hawapo kwa wakati mmoja, wanaweza kukwama kufikia baadhi ya uamuzi.

Mawaziri na manaibu wao katika kamati hiyo ni Christopher Chiza, Dk Kebwe Steven Kebwe, Mwigulu Nchemba, Godfrey Zambi na Adam Malima.

Waziri Mkuu Pinda alinukuliwa akisema watajitahidi kupunguza ruhusa za mawaziri kwenda nje ya Dodoma, lakini akasema suala hilo lina changamoto kubwa kwani lazima shughuli za Serikali ziendelee, haziwezi kulala wakati wote wa vikao vya Bunge Maalumu.

Pinda alisema baadhi ya shughuli za Serikali zilishapangwa tangu mwanzo, hivyo siyo rahisi kuahirishwa wala kufutwa kwani zinaweza kusababisha athari kubwa. Alitoa mfano wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe ambaye siyo rahisi kumnyima ruhusa kutokana na aina ya majukumu aliyonayo.

Kauli yake iliungwa mkono na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa ambaye alinukuliwa akitoa mfano kwamba yeye na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka watalazimika kwenda Bagamoyo kutatua mgogoro wa ardhi katika eneo kinakojengwa Chuo Kikuu cha Muhimbili na kwamba wasipofanya hivyo ujenzi huo utakwama.

Leo wajumbe wa Bunge Maalum wanaendelea kujadili Rasimu ya Katiba ikiwa ni siku ya pili.

CHANZO, GAZETI LA MWANANCHI

No comments:

Post a Comment